Saturday 12 December 2015

Maana ya nadharia na maana ya Fasihi



Maana ya nadharia na maana ya Fasihi.
Nadharia ni mfumo wa mawazo ya kifalsafa yanayoeleza kuhusu maisha ya mwanadamu na mazingira yake.

Wamitila (2003), anaeleza kuwa nadharia ni istilahi inayotumiwa kurejelea kauli au kaida za kijumla zinazotegemezwa kwenye uwazaji fulani.

Fasihi ni sanaa ya lugha inayotumia fani mbalimbali kutolea dhamira na maudhui yanayohusu maisha ya mwanadamu.

Wamitila (2003), anasema kuwa fasihi ni kazi za kisanaa au zilizotumia lugha kwa usanii na zinazowasilisha suala fulani pamoja kwa njia inayoathiri, kugusa na kuacha athari fulani katika maisha ya binadamu.

Kulingana na Mazrui na Syambo (1992), fasihi ni utumiaji wa lugha kisanaa kutubainia utaratibu wa maisha yetu.

Wafula na Njogu (2007), wanasema kuwa nadharia ya fasihi ni mwongozo unaomwezesha msomaji wa kazi ya fasihi kuifahamu kazi ya fasihi katikatika vipengele vyake vyote.

Nadharia ya fasihi ni mfumo wa mawazo ya kifalsafa ambayo hubainisha maisha ya binadamu na mazingira yake.
 

Sunday 16 December 2012

SARUFI FINYIZI


SARUFI FINYIZI
Maana ya sarufi finyizi
Sarufi finyizi ni nadharia ya kisarufi ambayo inaangazia utaratibu wa kuchunguza lugha ulio na unyumbufu wa mielekeo tofauti inayowezeshwa na ufinyizi wake. Sarufi finyizi imekuwa ikikua ndani ya nadharia ya hapo awali ya sarufi zalishi tangu miaka ya tisini. Hasa hujikita katika kueleza sifa za kijumla ambazo lugha ya mwanadamu huwa nazo.

Nadharia hii ilianzishwa na mwanaisimu wa Kimarekani na mwenye asili ya Uyahudi Noam Chomsky. Katika sarufi finyizi, Chomsky anaiwasilisha sio hasa kama nadharia bali kama utaratibu wa uchunguzi wa lugha. Nadharia hii ilijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka wa 1993 kupitia kazi yake Chomsky "A minimalist program for linguistic theory."
Hata hivyo, nadharia hii aliiweka wazi mwaka wa 1995 katika chapisho lake "The Minimalist Program." Baadhi ya watu waliowahi kuirejelea na kuizungumzia nadharia hii ni kama vile Webelhuth (Tah) (1995), Brody (1995), Cook na Newson (1996), Radford (1997) miongoni mwa wengine.
Sarufi finyizi ni maendelezo na uboreshaji wa nadharia ya sarufi zalishi iliyoanzishwa na Chomsky mwenyewe alipoizungumzia kwa mara ya kwanza mwaka wa 1957 katika chapisho lake “Syntactic Structures.’  
Sarufi zalishi ilianza hasa kwa kutofautisha dhana mbili kuu ambazo ni umilisi lugha na utendaji lugha. Pia ilitambulisha muundo nje na muundo ndani. Muundo ndani uliwakilisha umilisi nao muundo nje ukawakilsha utendaji.
Kufuatia sarufi finyizi, dhana ya muundo ndani iliondolewa ikabaki ile ya muundo nje pekee. Aidha vinadharia vilivyoongoza uchanganuzi wa sentensi viliondolewa na vikageuzwa kuwa kanuni za kisintaksia katika sarufi finyizi. Jambo hili linaangaliwa kuwa na umuhimu wa kuifanya nadharia ya lugha kuwa na uwekevu zaidi na urahisi kuliko sarufi panuzi ya awali.
Sarufi finyizi inajikita katika kuendeleza malengo ya sarufi zalishi ambayo yanahusisha kuandaa sintaksia bia ya lugha. Hii ina maana ya sarufi ambayo inajumlisha kanuni zinazoweza kudhihirika katika lugha yoyote ya mwanadamu. Hivyo basi, sarufi ya kijumla inayoeleza sifa zinazopatikana katika lugha zote za mwanadamu inazingatia maongozi maalum. Haya ni pamoja na sifa ya kuwa na ufafanuzi toshelevu, uasilia wa lugha inayochunguzwa, upekee wa lugha ya mwanadamu na ujumla wa tanzu zote za lugha. Pia utumiaji wa vipengee vichache vyenye utoshelevu (ufinyizi) na urahisi au wepesi wa kueleweka.
Aidha, sarufi finyizi inalenga kutafuta uhusiano kati ya nadharia ya isimu na tanzu nyinginezo za lugha kama vile miundo ya fasihi na falsafa ya lugha.
Nadharia ya sarufi finyizi inajikita katika imani kuwa kunayo idadi maalum ya sheria ambazo hufanya kazi kwa lugha zote za mwanadamu. Pia inashikilia kwamba kuna mseto wa sifa unaoweka msingi wa mfumo anaopata mtoto mzawa wa lugha fulani na ambao unamwezesha kuipata lugha kwa urahisi.
Chomsky (1995) anahoji kwamba yapo maswali yazuliwayo na sarufi finyizi tu ila majibu yake yanaweza kufafanuliwa katika nadharia yoyote. Kwake, swali muhimu zaidi kati ya yote ni lile linaloulizia sababu za lugha ya mwanadamu kuwa na sifa inazodhihirika kuwa nazo. Hivyo basi, sarufi finyizi inaandaa mtazamo mahsusi wa misingi ya sintaksia katika sarufi ya lugha. Katika hali hii, sarufi finyizi inapolinganishwa na mifumo mingineyo inatazamika kama nadharia.
Mhimili mwingine muhimu wa sarufi finyizi ni kuwa utendaji wa lugha miongoni mwa watu ni ishara tosha inyothibitisha mfumo komavu ulio na mpangilio maalum. Suala hili linaelekeza kwamba mfumo wa lugha umeingiliana na kurandana na kanuni nyepesi ya matumizi yake au kuhimiliwa ama na kiungo au kitivo fulani maalum katika ubongo wa binadamu.  Hii ni kumaanisha kwamba sarufi finyizi inajiegemeza katika dai eti sarufi bia inajumlisha muundo toshelevu unaofanikisha mahitaji ya ufahamu na yale ya kimatamshi.
 Katika mtazamo wa kinadharia na muktadha wa sarufi zalishi, sarufi finyizi inaainishwa kama mtazamo wa kanuni na sheria unaoangaliwa kuwa kielelezo cha upeo wa nadharia ambayo imekuwa ikikuzwa na kuendelezwa na isimu zalishi tangu miaka ya themanini. Mtazamo huu unachokieleza ni kuwepo kwa mseto maalum wa sheria zinazotumika katika lugha zote. Sheria hizi zikishirikishwa kwa miundo fulani ya kanuni zenye idadi mahsusi hueleza sifa za mfumo wa lugha ambao mtoto mzawa wa lugha hiyo huja kupata.
Sarufi finyizi inatambulisha jumla ya kategoria nane za maneno ambazo zinagawika katika matapo mawili. Tapo la kwanza ni lile la kileksia na la pili ni lile la kisarufi
Tapo la kileksia linahusisha kategoria za maneno ambazo zinawakilisha maana msingi au maana za kileksia. Kategoria hizi ni tano kama ifuatavyo:
i)            Nomino
ii)            Kitenzi
iii)          kivumishi
iv)          kielezi
v)            Kielezi

Tapo la kisarufi huwa na kategoria za maneno ambayo hayawakilishi maana ya kimsingi. Maneno haya huwa na umuhimu wa kuendeleza maana ya maneno ya kileksia. Kategoria hizi za kisarufi ni tatu:
i)           Kibainishi
ii)         Kishamirishi
iii)       Kipatanishi
.
Kutokana na maelezo haya,  ni wazi kuwa sarufi finyizi inatumika kufafanua na kuchanganua sentensi za Kiswahili. Sarufi finyizi inatambulisha sentensi sahili kama kishazi huru na kuchukulia utanzu wa sintaksia kuwa msingi zaidi.
Urahisishaji wa jinsi ya kuchanganua sentensi kwa kuondoa muundo ndani na muundo nje huenda una manufaa lakini itachukua muda kujenga uzoevu wa hatua zilizopendekezwa. Pia kuondolewa kwa vile vinadharia na kupunguzwa kumeondoa utata pamoja na kutupilia mbali dhana ya x-baa na ile nadharia ya utawala na ufungamanisho.
Japo sarufi finyizi ilipata uungwaji mkono na wasomi wanaisimu, kunao waliipinga mwishoni mwa miaka ya tisini. Kwa mfano, David E. Johnson na Shalom Lappin katika jarida la Natural Language and Linguistic Theory wanadai kuwa sarufi finyizi haikutokana na mtazamo wa kisayansi na hivyo haikuwa na malengo  yoyote ya kiusomi bali ni dhana iliyotokana na Chomsky kutaka tu kujidai na kunadhifisha nadharia ya awali ya lugha.
Wanadai kuwa kukubalika kwa sarufi finyizi hakukuwa na manufaa au ishara zozote za mapinduzi ya kisayansi katika isimu ila ni kutokana na nafasi na mchango wa hapo awali wa Chomsky katika taaluma  ya isimu.
Kutokana na hali ya nadharia hii kuendeleza sarufi bia, ni wazi kwamba sarufi finyizi hutumika kueleza vipengee vya lugha yoyote ya mwanadamu.

Mashairi na Uchambuzi wake


MASHAIRI
Maana:  - Shairi ni utungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum wa lugha ya mkato unaowasilisha mawazo au ujumbe kuhusu mwanadamu au mazingira yake na hufuata utaratibu fulani.

Migao ya mashairi
Mashairi huweza kugawika mara mbili.
i)                    Mashairi huru
ii)                  Mashairi ya arudhi

Mashairi ya arudhi
Huitwa pia mashairi ya kimapokeo. Haya ni mashairi yanayofuata kanuni za kimapokeo au arudhi za utunzi wa mashairi. Arudhi hizi ni pamoja na:
(i)                       Kugawika kwa shairi katika beti 
(ii)                     Beti kuwa na idadi maalum ya mishororo.
(iii)                   Mishororo ya ubeti kugawika katika vipande
(iv)                   Mishororo kuwa na ulinganifu wa mizani
(v)                     Shairi kuwa na urari wa vina
(vi)                   Shairi kuweza kuimbika / kuwa na mahadhi au mapigo.
(vii)                 Kuwepo kwa kipokeo katika shairi
(viii)               Kuwa na mtiririko wa mantiki na mawazo au muwala
(ix)                   Shairi kuwa na utoshelezo wa beti / kujisimamia kimaana.
Mashairi huru
Pia hujulikana kama mashairi ya kimapinduzi. Haya ni mashairi yasiozingatia lazima ya arudhi na hivyo huwa na muundo huru. Sifa zake kuu huweza kuwa:
a)      Lugha ya muhtasari
b)      Lugha yenye mahadhi
c)      Lugha ya kisanii iliyo na mafumbo na taswira
d)     Mara nyingine hugawika katika beti.
e)      Mishororo kamilifu (inayojitosheleza) na ile isiyo kamilifu (mishata)


SIFA ZA MASHAIRI
Mashairi huwa na sifa maalum zinazoyatambulisha kama kazi ya kishairi, yawe ya kimapokeo au kimapinduzi.
Sifa hizi ni kama vile:
1)            Mashairi hutumia lugha ya mkato / muhtasari
2)            Ni sanaa au kazi iliyobuniwa kwa ufundi
3)            Huwa na mpangilio maalum kuanzia mistari hadi beti.
4)       Hutumia lugha teule na msamiati teule uliosheheni tamathali, taswira na jazanda.
5)            Mashairi huwa na sifa ya kuweza kuimbika hivyo shairi ni wimbo na wimbo ni shairi.

Umuhimu / Dhima ya mashairi.
i)        Kupasha ujumbe  kwa hadhira kwa njia ya upole na mvuto
ii)      Kuelimisha na kuzindua jamii.
iii)    Kuendeleza na kukuza kipawa cha utunzi.
iv)    Kuhifadhi msamiati wa lugha ya Kiswahili na Sanaa ya fasihi.
v)      Kuburudisha hadhira na wasomaji.
     vi)  Kuwasilisha hisia za ndani za mtu na mawazo

 Uchambuzi wa Mashairi
Uchambuzi au uhakiki wa shairi ni kuvunjavunja shairi katika sehemu zake na kuzichunguza kwa makini ili kueleza ujumbe, dhamira, maudhui na hali ya vipengee vya shairi.
Uchambuzi wa mashairi huweza kufanywa kwa hatua.
Hatua za uchambuzi
i.                    Soma shairi polepole na makini kupata maana ya kijumla.
ii.                  Soma shairi tena kwa utaratibu ukizingatia maneno na vipande mbalimbali na kuchunguza maana ya  kila mojawapo.
iii.                Pitia maswali yote kwa makini ukitilia maanani aina ya majibu yanayotarajiwa.
iv.                Soma shairi tena ukipigia mstari kwa penseli sehemu zinazoelekea kujibu maswali.
v.                  Toa majibu kamilifu kulingana na swali kwa lugha ya mtiririko.

Vipengee vya Uchambuzi Wa Mashairi.
(i)                 Anwani  – Huwa ni muhtasari wa shairi katika neno au sentensi moja. Anwani ni kidokezo muhimu cha kinachozungumziwa katika shairi. Anwani huweza kuwa ya moja kwa moja, fumbo, kinaya, kibwagizo au sehemu ya kibwagizo.
          Ikiwa shairi halina anwani, basi lipewe anwani inayoafikiana na maudhui au dhamira kwa                      sentensi isiyozidi maneno 6.

(ii)        Maudhui – Haya ni masuala makuu au mambo muhimu yanayohusu mwanadamu au mazingira yake yanayozungumziwa katika shairi. Kwa mfano: malezi, siasa, usalama, unyanyasaji, ufisadi n.k
                         Maudhui hung’amuliwa kwa wepesi kutokana na kisa kilichomo katika shairi.

(iii)             Dhamira / shabaha - Ni lengo kuu la mshairi katika kusanifu utungo wake. Dhamira ya mtunzi huwa ni ujumbe kwa kifupi anaoutambua msomaji kutokana na mwelekeo wa usemaji wa mtunzi katika shairi. Mfano: Baada ya kusoma shairi, unaweza kung’amua mtunzi alitaka kusisitiza kauli kuwa uongozi mbaya haufai, misitu ni uhai n.k.
                        Dhamira hutokana na mwelekeo wa mawazo ya mshairi au falsafa yake.

(iv)       Mbinu na tamathali za lugha - Ni mbinu za uandishi na tamathali za usemi zilizotumiwa na mshairi  katika shairi.
            Mfano:
a)      Mazda / ziada / zidi - kurefusha maneno.    Mfano: enda kuwa enenda.
b)      Inksari / muhtasari - Ni kufupisha maneno. Mfano: aliyefika kuwa alofika.
c)      Utohozi – Mbinu ya kugeuza msamiati / maneno ya lugha geni ili yaandikike na kutamkika kana kwamba ni ya Kiswahili.         Mfano: Time - taimu
               One  – Wani
                                  Mbinu hii vilevile huitwa ukopaji au uswahilishaji.