SARUFI
FINYIZI
Maana
ya sarufi finyizi
Sarufi finyizi ni nadharia ya kisarufi
ambayo inaangazia utaratibu wa kuchunguza lugha ulio na unyumbufu wa mielekeo
tofauti inayowezeshwa na ufinyizi wake. Sarufi finyizi imekuwa ikikua ndani ya
nadharia ya hapo awali ya sarufi zalishi tangu miaka ya tisini. Hasa hujikita
katika kueleza sifa za kijumla ambazo lugha ya mwanadamu huwa nazo.
Nadharia hii
ilianzishwa na mwanaisimu wa Kimarekani na mwenye asili ya Uyahudi Noam
Chomsky. Katika sarufi finyizi, Chomsky anaiwasilisha sio hasa kama nadharia
bali kama utaratibu wa uchunguzi wa lugha. Nadharia hii ilijitokeza kwa mara ya
kwanza mwaka wa 1993 kupitia kazi yake Chomsky "A minimalist
program for linguistic theory."
Hata
hivyo, nadharia hii aliiweka wazi mwaka wa 1995 katika chapisho lake "The
Minimalist Program." Baadhi ya watu waliowahi kuirejelea na
kuizungumzia nadharia hii ni kama vile Webelhuth (Tah) (1995), Brody (1995), Cook na Newson (1996), Radford (1997)
miongoni mwa wengine.
Sarufi finyizi ni maendelezo na
uboreshaji wa nadharia ya sarufi zalishi iliyoanzishwa na Chomsky mwenyewe
alipoizungumzia kwa mara ya kwanza mwaka wa 1957 katika chapisho lake “Syntactic Structures.’
Sarufi zalishi ilianza hasa kwa
kutofautisha dhana mbili kuu ambazo ni umilisi lugha na utendaji lugha. Pia
ilitambulisha muundo nje na muundo ndani. Muundo ndani uliwakilisha umilisi nao
muundo nje ukawakilsha utendaji.
Kufuatia sarufi finyizi, dhana ya
muundo ndani iliondolewa ikabaki ile ya muundo nje pekee. Aidha vinadharia
vilivyoongoza uchanganuzi wa sentensi viliondolewa na vikageuzwa kuwa kanuni za
kisintaksia katika sarufi finyizi. Jambo hili linaangaliwa kuwa na umuhimu wa
kuifanya nadharia ya lugha kuwa na uwekevu zaidi na urahisi kuliko sarufi
panuzi ya awali.
Sarufi finyizi inajikita katika
kuendeleza malengo ya sarufi zalishi ambayo yanahusisha kuandaa sintaksia bia
ya lugha. Hii ina maana ya sarufi ambayo inajumlisha kanuni zinazoweza
kudhihirika katika lugha yoyote ya mwanadamu. Hivyo basi, sarufi ya kijumla inayoeleza
sifa zinazopatikana katika lugha zote za mwanadamu inazingatia maongozi maalum.
Haya ni pamoja na sifa ya kuwa na ufafanuzi toshelevu, uasilia wa lugha
inayochunguzwa, upekee wa lugha ya mwanadamu na ujumla wa tanzu zote za lugha.
Pia utumiaji wa vipengee vichache vyenye utoshelevu (ufinyizi) na urahisi au
wepesi wa kueleweka.
Aidha, sarufi finyizi inalenga
kutafuta uhusiano kati ya nadharia ya isimu na tanzu nyinginezo za lugha kama
vile miundo ya fasihi na falsafa ya lugha.
Nadharia ya sarufi finyizi
inajikita katika imani kuwa kunayo idadi maalum ya sheria ambazo hufanya kazi
kwa lugha zote za mwanadamu. Pia inashikilia kwamba kuna mseto wa sifa unaoweka
msingi wa mfumo anaopata mtoto mzawa wa lugha fulani na ambao unamwezesha
kuipata lugha kwa urahisi.
Chomsky (1995) anahoji kwamba yapo
maswali yazuliwayo na sarufi finyizi tu ila majibu yake yanaweza kufafanuliwa
katika nadharia yoyote. Kwake, swali muhimu zaidi kati ya yote ni lile
linaloulizia sababu za lugha ya mwanadamu kuwa na sifa inazodhihirika kuwa
nazo. Hivyo basi, sarufi finyizi inaandaa mtazamo mahsusi wa misingi ya
sintaksia katika sarufi ya lugha. Katika hali hii, sarufi finyizi
inapolinganishwa na mifumo mingineyo inatazamika kama nadharia.
Mhimili mwingine muhimu wa sarufi
finyizi ni kuwa utendaji wa lugha miongoni mwa watu ni ishara tosha
inyothibitisha mfumo komavu ulio na mpangilio maalum. Suala hili linaelekeza
kwamba mfumo wa lugha umeingiliana na kurandana na kanuni nyepesi ya matumizi
yake au kuhimiliwa ama na kiungo au kitivo fulani maalum katika ubongo wa
binadamu. Hii ni kumaanisha kwamba
sarufi finyizi inajiegemeza katika dai eti sarufi bia inajumlisha muundo
toshelevu unaofanikisha mahitaji ya ufahamu na yale ya kimatamshi.
Katika mtazamo wa kinadharia na muktadha wa sarufi
zalishi, sarufi finyizi inaainishwa kama mtazamo wa kanuni na sheria
unaoangaliwa kuwa kielelezo cha upeo wa nadharia ambayo imekuwa ikikuzwa na
kuendelezwa na isimu zalishi tangu miaka ya themanini. Mtazamo huu
unachokieleza ni kuwepo kwa mseto maalum wa sheria zinazotumika katika lugha
zote. Sheria hizi zikishirikishwa kwa miundo fulani ya kanuni zenye idadi
mahsusi hueleza sifa za mfumo wa lugha ambao mtoto mzawa wa lugha hiyo huja
kupata.
Sarufi finyizi inatambulisha jumla ya kategoria nane za maneno
ambazo zinagawika katika matapo mawili. Tapo la kwanza ni lile la kileksia na
la pili ni lile la kisarufi
Tapo la kileksia linahusisha kategoria za maneno ambazo
zinawakilisha maana msingi au maana za kileksia. Kategoria hizi ni tano kama
ifuatavyo:
i)
Nomino
ii)
Kitenzi
iii)
kivumishi
iv)
kielezi
v)
Kielezi
Tapo la kisarufi huwa na kategoria za maneno ambayo
hayawakilishi maana ya kimsingi. Maneno haya huwa na umuhimu wa kuendeleza
maana ya maneno ya kileksia. Kategoria hizi za kisarufi ni tatu:
i)
Kibainishi
ii)
Kishamirishi
iii) Kipatanishi
.
Kutokana
na maelezo haya, ni wazi kuwa sarufi finyizi inatumika
kufafanua na kuchanganua sentensi za Kiswahili. Sarufi finyizi inatambulisha
sentensi sahili kama kishazi huru na kuchukulia utanzu wa sintaksia kuwa msingi
zaidi.
Urahisishaji wa jinsi ya kuchanganua
sentensi kwa kuondoa muundo ndani na muundo nje huenda una manufaa lakini
itachukua muda kujenga uzoevu wa hatua zilizopendekezwa. Pia kuondolewa kwa
vile vinadharia na kupunguzwa kumeondoa utata pamoja na kutupilia mbali dhana
ya x-baa na ile nadharia ya utawala na ufungamanisho.
Japo sarufi finyizi ilipata
uungwaji mkono na wasomi wanaisimu, kunao waliipinga mwishoni mwa miaka ya
tisini. Kwa mfano, David E. Johnson na Shalom
Lappin katika jarida la Natural Language and Linguistic Theory wanadai kuwa sarufi finyizi
haikutokana na mtazamo wa kisayansi na hivyo haikuwa na malengo yoyote ya kiusomi bali ni dhana iliyotokana
na Chomsky kutaka tu kujidai na kunadhifisha nadharia ya awali ya lugha.
Wanadai
kuwa kukubalika kwa sarufi finyizi hakukuwa na manufaa au ishara zozote za
mapinduzi ya kisayansi katika isimu ila ni kutokana na nafasi na mchango wa
hapo awali wa Chomsky katika taaluma ya
isimu.
Kutokana na hali ya nadharia hii
kuendeleza sarufi bia, ni wazi kwamba sarufi finyizi hutumika kueleza vipengee
vya lugha yoyote ya mwanadamu.