NADHARIA YA
UPOKEZI/MWITIKIO WA MSOMAJI
Malengo
ya kazi hii ni:
(a) Kueleza maana ya nadharia ya upokezi.
(b) Kueleza historia fupi ya nadharia hii
pamoja na kuwataja waasisi wa nadharia hii.
(c) Kueleza mihimili ya nadharia hii.
I. UTANGULIZI
Nadharia inayoshughulikia upokeaji wa
matini za fasihi inahusiana na ulimbwende na mitazamo ya kisaikolojia. Kimapokeo, msomaji huwa na mawazo kuhusu
matini anayopitia. Kutokana na tajriba
ya usomaji, msomaji hupata hisi maalum.
Uteuzi na upokeaji wa sanaa hushirikishwa sana na hisi kwa mujibu imani
na nadharia za kilimbwende.
Ulimbwende
ni mwelekeo wa kusimulia ambapo wahusika walikuwa mashujaa na wenye nguvu za
ajabu na ambao walikuwa wanajeshi.
HISTORIA FUPI YA NADHARIA YA UPOKEZI NA
WAASISI WA NADHARIA YENYEWE
Nadharia hii
inayomweka msomaji katikati ya uhakiki wa fasihi ilianza miaka ya sitini na
sabini ya karne ya ishirini hasa kule Marekani na Ujerumani.
Waasisi na watetezi wakuu wa nadharia
hii ni Stanley Fish (1980), James Tompkins (1980), Wolfgang Iser (1974, 78)
Haus Robert Jauss, Roland Barthes na wengine.
Kwa mujibu wa wavuti wa Wikipedia, wananadharia wa upokezi wanaweza
kubainishwa katika makundi matatu:
(a) Wale
wanoangazia kwenye tajriba za kipekee za msomaji (Individualists). Hawa ni pamoja
na C. S. Lewis (1961), Stanley Fish (1967) na Norman Holland (1968) ambao walikuwa Wamarekani.
(b) Wale
wanaofanya majaribio ya kisaikolojia kwa kikundi maalum cha wasomaji (experimenters). Hawa ni Reuven Tsur, Richard Gerrig, David
Miall na Donald Kuiken.
(c) Wale
wanaochukulia kwamba wasomaji wote wataipokea kazi ya fasihi kwa njia
sawa. (Uniformists). Hawa
ni Wajerumani kama vile Wolfgang Iser na Haus Robert Jauss.
Hata hivyo,
Stanley Fish anadai kwamba sanaa ya maneno haichanganuliwi kwa kutumia mikakati
ya jaribio la kisayansi katika maabara.
Anasema kwamba jaribio la kisayansi huonyesha ujuzi uliofanikiwa au ujuzi ambao
haujafanikiwa. Anayefanya jaribio la
kisayansi huweka mpaka wa kihisia na kimawazo kati ya nafsi yake na jambo
linalomshughulisha.
MIHIMILI
YA NADHARIA YA UPOKEZI
Waitifaki wa
nadharia hii huuliza maswali ambayo kwayo misingi ya nadharia hii
imejengeka. Maswali haya ni:-
(a) Kuna uwiano wowote kati ya maana inayosomwa na jinsi msomaji
anavyoihakiki?
(b) Je, kila kazi ya fasihi ina maana
kufuatana na msomaji binafsi na jinsi anavyoichukulia?
(c) Kuna wasomaji ambao husoma na kufasiri
kazi za fasihi vizuri zaidi kuliko wasomaji wengine.
(d) Msomaji hutumia vigezo gani kujijulisha
iwapo mawazo yake juu ya kazi fulani yanafaa au
hayafai?
Adena Rosmarin katika (Murfin 1991)
anadai kuwa kazi ya fasihi ni kama kinyago ambacho
hakijakamilika na kwa hivyo mchongaji hujaribu kukikamilisha. Kwa hivyo, mhimili wa kwanza wa nadharia hii ni
kwamba:
(1) Msomaji huikamilisha kazi ya sanaa kwa
kuijaliza kwa usomaji makini au kuidhalilisha kwa
usomaji wa kiholela.
Iser na Fish wanadai kwamba kazi ya
fasihi huwa na mapengo mengi ambayo msomaji hulazimika
kuyajaliza. Kwa hivyo, msomaji
hushurutika kutunga matini mpya ambazo zimechochewa
kuzalika kutokana na matini asili
zilizoko kwenye kurasa.
(2) Nadharia hii inasisitiza athari za kazi
za fasihi juu ya akili na maarifa ya mwandishi.
Wasomaji mbalimbali
hufasiri athari hizi kupitia njia tofauti tofauti kutengemea:
(i) Tofauti
kati ya matini na hisia za kibinafsi za msomaji.
(ii) Namna
matini inavyoelekezea au kutatiza mwitikio wa msomaji. Sifa inayozua usomaji
mzuri au mbaya wa kazi inayohusika.
(3) Wanadhania hawa wanashikilia kuwa kuna
njia mbili za kusoma kazi ya fasihi ambazo ni:
(i) Njia
inayofafanua na kusisitiza mawazo ambayo kitambo yamejulikana na kutambuliwa
na msomaji.
(ii) Kuwasilisha
kazi ya fasihi kimafumbo ili kumchochea msomaji kujitafutia na kujiamulia ujumbe uliomo katika kazi anayoisoma. Kwa hivyo mafumbo hayo yanapaswa kusomwa
mara kadhaa ili msomaji aelewe matini anayosoma.
(4) Usomaji ni tendo linalofanyika na
kutekelezwa kwa wakati maalum, kwamba wakati wa kusomwa kwa matini huathiri maana ya matini hiyo. Fish anadai kwamba wasomaji wanapasa kufanya mikataba ya aina
fulani na matini hizi katika miktadha mbalimbali.
(5) Msomaji anayetumia mkakati wa mwitikio
kusoma kazi ya sanaa hufuata hatua tatu katika
weledi wa kazi za fasihi.
(i) Hurejelea
kazi inayosomwa kwa tafsiri ili ithibitishwe kwamba kazi hiyo inaafikiana na yale yanayokumbukwa na msomaji.
(ii) Hubainisha
jinsi miktadha ya matini isiyohusiana moja kwa moja na maandishi inavyoweza kuhusishwa na kutangamanishwa na msomaji.
(iii) Hudhihirisha kuwa maoni ya msomaji yanafungamana na mada
muhimu za hadithi.
(6) Madharia hii inazingatia usomaji,
msomaji na upokezi. Huck (1976) anadai
kuwa lengo kuu hapa ni kuwabainisha wasomaji, kuwachunguza pamoja na tendo
zima la usomaji. Kwake mvuto wa watoto kwa sanaa ni kigezo muhimu katika
kutathmini ubora wa kitabu cha watoto. Naye
Louis Rosenblatt (1938) katika kitabu chake Literature and Exploration
anasema kuwa ni muhimu kwa mwalimu kuepuka kulazimisha kasumba au misimamo fulani ya jinsi wanafunzi
wanapaswa kuipokea kazi fulani ya fasihi.
HITIMISHO
Baadhi ya
wahakiki wa kisasa wanadai kwamba uhakiki kwa mujibu wa nadharia ya upokezi
umekosa kutambua kuwa matini ina uwezo wa kupanua kuelewa kwa msomaji. Aidha, wanadai kwamba nadharia hii
imewaruhusu wasomaji kufasiri matini/kazi ya fasihi jinsi wapendavyo. Maoni yetu hapa yanaafiki yale ya Iser (1976)
aliposisitiza kuwa msomaji hana budi kuzielewa mbinu, kaida na kanuni
zinazotumiwa katika kazi fulani ya fasihi ili kuweza kuisoma kikamilifu. Kwa hivyo, nadharia hii ingali muhimu katika
uhakiki wa kazi za fasihi kwa jumla.
MAREJELEO
Bennet,
Andrew (1995). Readers and Reading. London
& New York. Longman.
Daiches,
David (1981) Critical Approaches to
Literature. London: Longman.
Kimani
Njogu et. al (1999) Ufundishaji wa
Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi:
Jomo Kenyatta.
Tompkins,
Jane (1980). Reader – Response Criticism.
Baltimore and London: John Hopkins
Wafula,
R. M & Kamau Njogu (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
Wamitila,
K. W (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus
Books.
No comments:
Post a Comment